Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtimua kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG), Othman Masoud Othman.
Hatua hiyo ya Dk Shein imekuja ikiwa ni wiki moja
tangu mwanasheria huyo kukataa ibara 22 za Katiba inayopendekezwa wakati
wa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi
Zanzibar, Dk Abdulhamid Yahya Mzee imesema Rais Shein amempandisha cheo
aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu, Said Hassan Said kuwa AG.
“Amefanya mabadiliko hayo kwa mamlaka aliyopewa na
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Ibara ya 55(1), 53, 54(1) na
55(3)... Rais Shein ametumia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011,
Kifungu cha 12(3) na 27,” ilisema taarifa hiyo.
Othman ambaye hivi karibuni alijiondoa katika
Kamati ya Uandishi ya lililokuwa Bunge Maalumu kwa kutoridhika na baadhi
ya mambo, alieleza bungeni kutokubaliana na ibara ya pili, tisa, 86,
37, 70 hadi 75 na Sura ya 11 ambayo ina ibara ya 158 hadi 161, Sura ya
16 yenye ibara za 243 hadi 251 na Nyongeza ya Kwanza inayozungumzia
mambo ya Muungano.
Hatua hiyo ilionekana kuwaudhi baadhi ya wajumbe
ambao walimzomea na baada ya Bunge kuahirishwa, alitolewa kupitia mlango
wa nyuma wa Ukumbi wa Bunge chini ya ulinzi mkali.
Baadaye Othman alisema kwamba licha
ya kuwa yeye ni Mwanasheria Mkuu wa SMZ, alitumia utashi wake wa
kidemokrasia kupiga kura kuzikataa ibara hizo, kutokana na kutoridhishwa
na jinsi zilivyoandikwa.
“Katika suala la Katiba, Serikali ilishatamka
kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kwamba haina msimamo.
Ndiyo maana uliona misimamo ilikuwa imeachwa kwenye vyama vya siasa,
mimi siyo Mwanasheria Mkuu wa chama chochote.
“Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa maana ya upande… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu.”
Ibara alizozikataa
Ibara ya 2. Hii inazungumzia eneo la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, likiwamo la Tanzania Bara na la Zanzibar pamoja na
madaraka ya rais wa Jamhuri kugawa eneo lolote la nchi katika mikoa.
Ibara ya 9 inayoeleza ukuu wa Katiba yenyewe na kuwa ndiyo
sheria kuu. Inazuia kutungwa kwa sheria yoyote inayotofautiana nayo na
inaelekeza wananchi na taasisi zote kuitii.
Sura ya Saba (Ibara 70-75). Hizi zinahusu muundo
wa muungano na mgawanyo wa majukumu na mamlaka ya Serikali za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na SMZ.
Pia ibara hizo zinafafanua wajibu wa viongozi
wakuu katika kuhakikisha kuwa wanatetea, wanalinda, wanaimarisha na
kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara ya 86 na 87 inayofafanua utaratibu wa
uchaguzi wa rais wa Muungano na taratibu za kisheria kwa mgombea
asiyeridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu kupinga uchaguzi huo
mahakamani.
Ibara ya 128. Hii inahusu mamlaka ya Bunge la
Muungano na Baraza la Wawakilishi katika kutunga sheria na kuzuia Baraza
la Wawakilishi kutunga sheria juu ya jambo lolote ambalo liko chini ya
mamlaka ya Bunge na kulizuia Bunge kutunga sheria kuhusu jambo lililoko
chini ya Baraza la Wawakilishi.
Ibara za 159, 160, 161 zinazozungumzia Rais wa
Zanzibar na majukumu yake, Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar pamoja na majukumu yake.
Sura ya 16 (243-251). Hizo zinahusu Mfuko Mkuu wa
Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano. Misingi ya matumizi ya fedha za
umma, misingi inayoongoza matumizi ya fedha za Muungano, akaunti ya
fedha ya pamoja, mfuko wa hazina na masharti ya kutoa fedha za matumizi
katika mfuko huo.
Pia sura hiyo inaweka utaratibu wa kuidhinisha
matumizi ya fedha kabla ya sheria inayohusu matumizi ya fedha ya
Serikali, mfuko wa matumizi ya dharura na ulipaji wa mishahara ya baadhi
ya watumishi.
Nyongeza ya Kwanza. Hii ni orodha ya mambo ya Muungano ambayo yameongezwa kutoka saba ya Rasimu ya Warioba kuwa 14.
Mwanasheria Mkuu mpya wa Zanzibar, Mhe Said Hassan Said