Monday, October 6, 2014

JWTZ yamtimua kazi askari

Jeshi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha nchi kavu, limemfukuza kazi askari wake wa Kikosi 128 KJ cha Nyandoto, baada ya kudaiwa kuhusika katika tukio la kurushiana risasi na Polisi wa Kituo cha Stendi, wilayani Tarime.
Mbali na hatua hiyo, pia JWTZ imelaani kitendo hicho na kutaka hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya mwanajeshi huyo kutokana na kukiuka taratibu za kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu, Bregedia Jenerali Mathew Sukambi alisema askari huyo ambaye hata hivyo hakumtaja jina, alisema amekiuka kiapo cha jeshi, hivyo hastahili kuwa askari tena.
“Naomba niseme, askari huyu aliyeshiriki kwenye tukio hilo lililotokea Oktoba 3, hastahili tena kuwa askari wa JWTZ, kwani amekiuka kiapo cha jeshi,” alisema Sukambi na kuongeza: “Taratibu za jeshi zinaagiza kuwa watiifu na nidhamu ya hali ya juu, hivyo kwa kitendo chake ni wazi siyo mtiifu.”
Alisema wananchi watambue kuwa jeshi halikumtuma askari huyo kufanya kitendo hicho na kwamba amekifanya yeye binafsi.
Bregedia Jenerali Sukambi aliagiza sheria zichukuliwe dhidi ya askari huyo sambamba na wote alioshirikina nao.
Tukio hilo la kurushiana rasasi na askari polisi, lilitokea Oktoba 3 mwaka huu, wilayani Tarime na kusababisha watu 12 kujeruhiwa. Sababu ya mtafaruku huo ni baada ya wanajeshi kujaribu kumchukua mwenzao aliyekamatwa na trafiki kwa kosa la kundesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu.

No comments:

WELCOME TO SEEISSAI BLOG